Tajiri zaidi barani Afrika na Mnigeria Aliko Dangote baada ya kupitia changamoto za VISA hata pale anapotaka kusafiri ndani ya Bara lake la Afrika alikowekeza Mabilioni ya dola kwenye biashara mbalimbali, amelalamikia kukumbana na vikwazo vingi zaidi anaposafiri barani Afrika kuliko hata Wageni walio na passport za Ulaya.
Dangote aliyasema haya kwenye mjadala wa Jukwaa la Wakurugenzi Watendaji kutoka Bara la Afrika uliofanyika hivi karibuni Kigali, Rwanda ambapo amenukuliwa akisema “Kama mwekezaji, kama mtu ambaye anataka kuifanya Afrika kuwa kubwa, inabidi niombe visa 35 tofauti kwa kutumia pasipoti yangu”.
Changamoto za utapatikanaji wa vibali vya kusafiria kwa Bilionea Dangote (67) zilizua hisia zisizo nzuri kuhusu kukatishwa tamaa kwa Raia mbalimbali wa Afrika pale wanapotaka kusafiri ndani ya Bara lao katika jukwaa hilo la ‘Africa CEO Forum’ ambako Dangote aliipongeza Rwanda ambayo ilitangaza kuondoa VISA kwa Raia wote wa Afrika mwaka wa 2023 huku Nchi nyingine kama Benin, Gambia na SheliSheli pia zikifanya kama ilivyofanya Rwanda.
Kwa upande mwingine Umoja wa Afrika (A.U) umesema moja ya malengo yake ni kuondoa vikwazo vya Waafrika kusafiri, kufanya kazi na kuishi ndani ya Bara lao kwa kubadilisha sheria za vikwazo na kukuza usafiri bila VISA japokuwa utekelezaji wake umekuwa ukisogea taratibu.