Vilabu vya Premier League vilitumia rekodi ya pauni bilioni 2.36 katika dirisha la usajili la majira ya kiangazi lilipofungwa Ijumaa kwa msururu wa mikataba iliyochelewa.
Brighton, Burnley, Chelsea, Everton, Liverpool, Nottingham Forest, Manchester City, Manchester United na Tottenham ni miongoni mwa klabu za ligi kuu ambazo zote zilipata dili za kuchelewa.
Man City walihusika katika mikataba miwili mikubwa zaidi ya siku ya mwisho, kumsajili Matheus Nunes kutoka Wolves kwa £53m na kumuuza Cole Palmer kwenda Chelsea kwa £45m.
Tottenham ilitumia pesa nyingi dakika za mwisho za dirisha kwa kumnasa Brennan Johnson kutoka Forest kwa dau la pauni milioni 47.5.
Forest ndiyo klabu yenye shughuli nyingi zaidi siku ya mwisho kwani hawakupoteza muda kuwekeza pesa za Johnson.
Beki Nuno Tavares aliwasili kwa mkopo kutoka Arsenal, kiungo wa Argentina Nicolas Dominguez alijiunga kutoka Bologna huku Remo Freuler akienda kinyume, huku winga Callum Hudson-Odoi na kipa Odysseas Vlachodimos wakisajiliwa kutoka Chelsea na Benfica mtawalia.
Ibrahim Sangare aliwasili City Ground kwa mkataba wa miaka mitano kutoka PSV na mshambuliaji wa zamani wa Liverpool Divock Origi alijiunga kwa mkopo kutoka AC Milan.
Liverpool – ambao wamekataa ofa ya pauni milioni 150 kwa Mohamed Salah kutoka kwa Al-Ittihad ya Saudi Arabia Pro League – na Manchester United wote waliongeza kwenye idara zao za kiungo, huku mchezaji wa kimataifa wa Uholanzi Ryan Gravenberch akikamilisha uhamisho wa pauni milioni 35 kwenda Anfield kutoka Bayern Munich.
United ilimsajili Sofyan Amrabat kutoka Fiorentina kwa mkopo, huku pia ilimpata mlinda mlango wa kimataifa wa Uturuki Altay Bayindir kutoka Fenerbahce, beki wa kushoto Sergoo Reguilon kwa mkopo kutoka Tottenham hadi Juni 2024 na Jonny Evans kwa mkataba wa mwaka mmoja.
United pia ilimtoa Mason Greenwood kwenda Getafe kwa mkopo wa msimu mzima baada ya kutangaza mwezi uliopita kuwa hataichezea klabu hiyo tena.