Viongozi wa nchi saba tajiri duniani leo wanaanza mkutano wao wa siku tatu kwenye kaunti ya Cornwall nchini Uingereza kujadili masuala kadhaa ikiwa pamoja na janga la maambukizo ya virusi vya corona, juhudi za kufufua uchumi, mabadiliko ya tabia nchi na siasa za dunia.
Viongozi wa nchi hizo maarufu kama G7 tayari wameshaahidi kutoa msaada wa dozi bilioni moja za chanjo kwa nchi zinazoendelea ili kupambana na maambukizi ya virusi vya corona.
Nchi hizo saba ni pamoja na Marekani, Ujerumani, mwenyeji wa mkutano huo Uingereza na Canada. Nyingine ni Ufaransa, Japan na Italia. Viongozi kutoka Korea Kusini, Afrika Kusini na Australia pia wanashiriki kwenye mkutano huo na India pia itashiriki lakini kwa njia ya video.