Wajumbe wa Baraza la Kitaifa la Ushauri la Somalia wamekubali kuendelea na mashambulizi makubwa ya kijeshi dhidi ya kundi la wanamgambo wa al-Shabab wenye mafungamano na al-Qaeda yaliyoanza Agosti mwaka jana.
Baraza hilo ambalo linawaleta pamoja viongozi wa serikali ya shirikisho na majimbo ya kikanda, lilikutana katika mji wa kati wa Dhusamareb siku ya Jumapili kujadili mapambano dhidi ya kundi hilo.
Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa X (zamani ikijulikana kama Twitter), ofisi ya rais ilisema viongozi hao walikubaliana kuratibu mashambulizi hayo na “kuoanisha na mkakati wa kitaifa wa kukabiliana na ugaidi” ili kukomesha uasi wa muda mrefu wa kundi hilo.
Viongozi hao walisema wataunda “muundo wa pamoja wa amri” kusimamia operesheni za kijeshi dhidi ya wanamgambo.
Mkutano huo umekuja saa chache baada ya jeshi kuteka ngome kuu ya al-Shabab katika eneo la kati la Galgudud, katika kile ambacho vyombo vya habari vya ndani vilieleza kuwa ni pigo kubwa kwa kundi hilo
Rais Hassan Sheikh Mohamud ameapa kulishinda kundi hilo kabla ya mwisho wa 2023.