Marais hao wa Uganda na Zimbabwe walikutana na mwenzao wa Urusi Vladimir Putin siku ya Alhamisi, pembezoni mwa Mkutano wa wakuu wa Urusi na Afrika huko Saint Petersburg.
Kiongozi huyo wa Urusi alisema kuwa maendeleo ya uhusiano na nchi za Afrika ni “moja ya vipaumbele visivyoweza kubadilika” vya Shirikisho la Urusi, akizungumza wakati wa mazungumzo ya pande mbili na Rais wa Uganda Yoweri Museveni.
Putin amekuwa akifanya mikutano ya nchi mbili na viongozi wa Afrika wakati wa mkutano huo wa siku mbili, wa pili tangu 2019.
Idadi ya wakuu wa nchi imepungua kutoka 43 mwaka 2019 hadi 17 sasa, huku wajumbe wa nchi 49 wakihudhuria. Ikulu ya Kremlin imelaani kile ilichokiita shinikizo chafu la Magharibi la kukatisha tamaa mataifa ya Afrika kushiriki.
Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa alionyesha kuunga mkono hatua za Urusi nchini Ukraine, akisema, “Niruhusu niseme binafsi kwamba Zimbabwe iko katika mshikamano na Shirikisho la Urusi katika operesheni maalum ya kijeshi ya nchi yako nchini Ukraine.”
Nchi za Kiafrika zimesalia kugawanyika kuhusu vita vya Ukraine.
Mataifa 54 ya bara hilo yanaunda kambi kubwa zaidi ya upigaji kura katika Umoja wa Mataifa na yamegawanyika kuliko kanda nyingine yoyote kuhusu maazimio ya Baraza Kuu yanayokosoa vitendo vya Urusi nchini Ukraine.
Zimbabwe ni mojawapo ya nchi 17 za Kiafrika ambazo zilijizuia kupiga kura kuhusu azimio la Umoja wa Mataifa la mwaka 2022 lililotaka wanajeshi wa Urusi waondoke.