Viongozi wakuu wa taifa, rais William Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua, wameelezea masikitiko yao kufuatia habari za kusikitisha za kisa cha moto kilichogharimu maisha ya wanafunzi 17 katika shule ya Hillside Endarasha Academy eneo bunge la Kieni, kaunti ya Nyeri.
Habari zilizogonga vichwa vya habari vya vituo vyote vya habari nchini Kenya ziliripoti kuwa wanafunzi wengine kadhaa walipata majeraha ya moto katika tukio hilo la kuhuzunisha lililotokea Alhamisi usiku.
Huku akiomboleza wafu na kuwafariji waliojeruhiwa, rais Ruto alihakikishia familia zilizoathirika sapoti ya serikali katika nyakati hizi za huzuni.
“Mawazo yetu yako kwa familia za watoto ambao wamepoteza maisha katika mkasa wa moto katika Chuo cha Hillside Endarasha katika Kaunti ya Nyeri,” Rais Ruto alisema kwenye taarifa Ijumaa asubuhi.
Aliongeza, “Hizi ni habari za kuhuzunisha. Tunawaombea manusura wapone haraka.”
Kufuatia tukio hilo la kusikitisha, kiongozi huyo wa taifa sasa ameziagiza mamlaka husika kuchunguza kwa kina tukio hilo la kutisha na kuhakikisha waliohusika wanaadhibiwa.
“Serikali chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani na Uratibu wa Serikali ya Kitaifa inakusanya rasilimali zote muhimu ili kusaidia familia zilizoathirika. Poleni sana,” Ruto alisema.
Katika taarifa yake, naibu wa rais Rigathi Gachagua alitoa rambirambi kwa familia za wanafunzi waliofariki na kuwatakia ahueni ya haraka waliojeruhiwa.
Pia alizitaka shule kutekeleza hatua za ulinzi na usalama ili kuwalinda wanafunzi wao.
“Tunaungana na familia, shule na nchi nzima kuomboleza roho hizi za vijana walioaga. Tunawaombea ahueni ya haraka manusura wa moto huu wa moto. Mungu azipe familia ujasiri wa kustahimili msiba huo,” Gachagua alisema.
Aliongeza, “Tunaomba shule kutekeleza hatua za usalama na usalama kama ilivyoainishwa na Wizara ya Elimu na mashirika mengine ili kuzuia matukio kama haya.”