Rais wa Kenya, William Ruto ametangaza kwamba raia wa kigeni wanaoingia nchini humo hawatahitajika kuwa na visa kuanzia mwezi Januari, mwaka ujao.
Akihutubia wakati wa maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa nchi hiyo hapo jana jijini Nairobi, rais Ruto amesema hatua hiyo inalenga kuboresha sekta ya utalii nchini humo. Amesema ili kutekeleza sera ya kutohitaji visa, serikali imeandaa jukwaa la kidijitali ili kuhakikisha kuwa wageni wanaoingia nchini humo wanatambuliwa kabla kupitia jukwaa la kielektroniki.
Katika hotuba yake, rais Ruto amesema utawala wake umejikita katika kufufua sekta muhimu za uchumi, ikiwemo uzalishaji, kilimo, afya, na huduma za kifedha kuendana na mfumo wa ukuaji unaohusisha watu.
Tangu alipoingia madarakani mwaka jana, Rais Ruto alipendekeza kuondolewa kwa visa kwa Waafrika wanaotembelea Kenya ili kutimiza ajenda ya maingiliano ya bara hilo.