Mizozo imekwamisha juhudi za kuwachanja watoto kote ulimwenguni, viongozi wa afya wameonya, kwani takwimu mpya zilionyesha takriban watoto milioni 14.5 hawajapokea dozi moja ya chanjo.
Zaidi ya nusu ya watoto hao wanaishi katika nchi ambako mizozo ya silaha au majanga mengine ya kibinadamu yamesababisha hali tete na hatarishi, kulingana na data kutoka kwa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, Unicef, na Shirika la Afya Ulimwenguni.
Vita nchini Sudan vimesababisha ongezeko kubwa la idadi ya watoto ambao hawajachanjwa, kutoka takriban 110,000 mwaka 2021 hadi wastani wa 701,000 mwaka jana. Yemen ina watoto 580,000 ambao hawajachanjwa, kutoka 424,000 miaka mitatu iliyopita.
Mbali na watoto milioni 14.5 wa “dozi sifuri” mnamo 2023, watoto milioni 6.5 “walichanjwa chini ya chanjo”, kumaanisha kuwa walikuwa hawajapokea dozi zao zote zilizopendekezwa.