Mtandao wa Wanawake, Katiba, Uchaguzi na Uongozi umetoa tamko la kulaani na kutaka hatua stahiki zichukuliwe juu ya tukio la Wanawake wakongwe kuchapwa viboko mkoani Tabora kwa tuhuma za uchawi.
Tamko la mtandao huo linakuja ikiwa ni siku chache baada ya kusambaa kwa taarifa ya kwamba Diwani wa Kata ya Kasisi, wilayani Urambo mkoani Tabora, Macho Salehe amewachapa viboko Wanawake wakongwe kwa shutuma za kujishughulisha na masuala ya uchawi na ushirikina.
Katika tamko hilo lililotolewa na Mkurugenzi wa WFT, Rose Marandu amesema..”Pamoja na kuipongeza Serikali kwa hatua ilizozichukua kufuatilia suala hili kupitia Wizara Maendeleo ya Jamii, l bado tunaona haja ya suala hili kuwekewa msisitizo na hatua madhubuti kuchukuliwa dhidi ya wanaokwamisha zoezi la upatikanaji wa haki kwa ukatili mkubwa uliotendeka,”.
“Hivyo basi, Mtandao wa Wanawake unalaani kitendo hicho na tunatoa wito kwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, TAMISEMI, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na Jeshi la Polisi kuchukua hatua stahiki ikiwa ni pamoja na kufanya upelelezi kwa wale wote waliohusika katika tukio hili la kinyama na la kusikitisha,”.
Pia mtandao huo umeshauri suala hilo lifuatiliwe na kushughulikiwa kwa uwazi ili wananchi wote waweze kurejesha imani ya utawala wa sheria na upatikanaji wa haki kwa viongozi na serikali kwa ujumla.
Hata hivyo, tayari Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dr.Doroth Gwajima ametoa maagizo ya wahusika wote kufuatiliwa sambamba na kufikishwa katika vyombo vya sheria.