Mahakama ya juu ya Urusi imetangaza kile inachokiita “vuguvugu la kimataifa la LGBT” kuwa shirika lenye msimamo mkali na kupiga marufuku shughuli zake kote nchini.
Uamuzi huo ulichochewa na hoja kutoka kwa wizara ya haki, ingawa hakuna shirika kama hilo lililopo kama taasisi ya kisheria.
Kesi hiyo ilisikilizwa kwa faragha, lakini waandishi wa habari waliruhusiwa kusikiliza uamuzi wa mahakama.
Hakuna mtu kutoka “upande wa mshtakiwa” aliyekuwepo, mahakama ilisema. Katiba ya Urusi ilibadilishwa miaka mitatu iliyopita ili kuweka wazi kuwa ndoa ina maana ya muungano kati ya mwanaume na mwanamke.
Muungano wa watu wa jinsia moja hautambuliwi hapa.
Kabla ya uamuzi huo, nilimuuliza Sergei Troshin, naibu wa manispaa ya St Petersburg ambaye alijitokeza akieleza kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja mwaka jana, kuwa hatua hiyo ina athari gani.
“Nadhani hii itamaanisha kwamba mtu yeyote ambaye serikali inamwona kuwa mwanaharakati wa LGBT anaweza kupata kifungo cha muda mrefu kwa ‘kushiriki katika shirika lenye itikadi kali’,” alisema. “Kwa mratibu wa kikundi kama hicho, kifungo kitakuwa cha muda mrefu zaidi.