Naibu Mrajisi wa Vyama vya Ushirika Usimamizi na Udhibiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Collins Nyakunga ametoa wito kwa Viongozi na Watendaji wa Vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS) kuwa na uelewa wa Sheria ya Vyama vya Ushirika Na.6 ya mwaka 2013, Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha Na.10 ya mwaka 2018, miongozo na Kanuni husika za Ushirika.
Mrajis ametoa wito huo akiongea na Viongozi pamoja na Watendaji wa Vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS) wakati wa mafunzo ya Sheria Na.10 ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018 iliyofanyika DSM.
Akizungumzia Uchaguzi katika Vyama vya Ushirika Mrajis amewakumbusha Viongozi na Watendaji kuzingatia suala la kufanya Chaguzi za Viongozi wa Vyama kwa mujibu wa Sheria, inayoelekeza Vyama kufanya Chaguzi kila baada ya miaka mitatu ya uongozi, amesisitiza kufanya Chaguzi na kupata viongozi wapya ni njia bora ya kuwajengea uwezo wengine katika uongozi, kukuza vipaji na kuhakikisha uendelevu wa vyama, amevita Vyama vyote vinavyopaswa kufanya chaguzi kutekeleza wajibu huo kwa mujibu wa taratibu ifikapo tarehe 30/06/2020.
Kaimu Meneja wa TRA SACCOS Bw. Joseph Wilbert amesema Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018 inaenda kuleta tija zaidi kwa vyama vya Ushirika hususani Vyama vya Akiba na Mikopo kutokana na maelekezo ya usimamizi wa rasilimali za Vyama. Akiongeza kuwa Mafunzo hayo yaliyotolewa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) yataongeza uwajibikaji kwa Vyama kwani yamewapa uelewa wa haki na Wajibu wao kama watendaji wa Vyama vya Ushirika.