Watu watano akiwemo Oscar Mariselian maarufu Wizkid (30), mkazi wa Nkuungu Dodoma Wizkid wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashitaka ya kuchapisha picha za ngono kupitia mtandao wa WhatsApp.
Mbali na Wizkid, washitakiwa wengine katika kesi hiyo namba 97/2019 ni Willium Kimaro (35), Doa Godfrey (36), mfanyabiashara, Feisal Mohammed (27) mkazi wa Ilala, Adulrahman Muhidin (34) mkazi wa Temeke Dar es Salaam ambaye ni Ofisa Usafirishaji.
Washitakiwa hao wamesomewa mashitaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Augustina Mmbando.
Akisoma mashitaka hayo, Wakili wa Serikali, Jenipher Masue amedai kuwa kila mshitakiwa anakabiliwa na shitaka moja kinyume na Sheria ya Makosa ya Mtandao kifungu namba 14 (1) (a) na kifungu cha (2) (a) namba 14 ya mwaka 2015.
Masue alidai kuwa washitakiwa walitenda makosa hayo Aprili 4 na 5, 2016 maeneo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alidai Aprili 4, 2016 Mariselian(Wizkid) alichapisha picha za ngono kupitia mtandao wa WhatsApp huku akijua kuwa ni kinyume na sheria.
Pia alidai Aprili 4, 2016 washitakiwa Kimaro, Godfrey, Mohammed na Muhidin walichapisha picha chafu kupitia mtandao huo ambazo ni kinyume na sheria hiyo.
Washitakiwa hao walikana mashitaka na upande wa mashitaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu Mmbando aliwataka washitakiwa kila mmoja kuwa na mdhamini mmoja kutoka taasisi inayotambulika mwenye kitambulisho ambaye atasaini bondi ya Sh milioni tano.
Washitakiwa hao walitimiza masharti ya kuachiwa kwa dhamana na Hakimu Mmbando aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 9,2019 kwa ajili ya kutajwa.