Polisi wamewakamata zaidi ya waandamanaji 200 waliokuwa wakipinga vita vya Israel dhidi ya Palestina nje ya Soko la Hisa la New York, wakidai kusitishwa kwa msaada wa kijeshi wa Marekani kwa Israel huko Gaza.
Waandamanaji hao walioshirikiana na makundi ya wanaharakati kama Jewish Voice for Peace, walikusanyika kwa wingi wakipaza sauti “Acha Gaza iishi” na “Sitisheni ufadhili wa mauaji ya kimbari” karibu na jengo maarufu la soko hilo la hisa.
Kwa mujibu wa msemaji wa polisi, jumla ya andamanaji 206 walikamatwa baada ya kuvuka uzio wa usalama uliowekwa mbele ya jengo kuu, ingawa hakuna aliyeingia ndani ya soko hilo.
Waandamanaji walielekeza hasira zao kwa kampuni za kutengeneza silaha na wakandarasi wa kijeshi wa Marekani kwa kuendelea kunufaika na migogoro hiyo.
Kundi la Jewish Voice for Peace lilitoa tamko kupitia mtandao wa X, likisema “Mamia ya Wayahudi na marafiki zao wamefunga Soko la Hisa la New York ili kudai Marekani isitishe uuzaji wa silaha kwa Israel na kunufaika na mauaji ya kimbari.”
Mauaji hayo yanaendelea kuleta hasira huku taarifa zikionesha kuwa zaidi ya Wapalestina 42,200, wakiwemo wanawake na watoto, wamepoteza maisha kutokana na mashambulizi ya Israel, huku pia ikiripotiwa mauaji mengine ya zaidi ya watu 2,000 nchini Lebanon.