Taasisi ya Waandishi Wasio na Mipaka (RSF) imefungua kesi ya uhalifu katika Mahakama ya Ujerumani dhidi ya Mwanamfalme Mohammed bin Salman ya uhalifu dhidi ya binadamu kutokana na mauaji ya Mwandishi wa Habari, Jamal Khashoggi.
Mashtaka hayo yanayotaka uchunguzi chini ya Sheria za Kimataifa za Ujerumani, yanaituhumu Saudi Arabia kuendesha mauaji ya Khashoggi ambaye aliuawa katika Ofisi za Ubalozi za Saudi Arabia Jijini Istanbul Oktoba mwaka 2018.
Marekani ilitoa ripoti ya kijasusi ambayo inaonesha Mwanamfalme Mohammed aliidhinisha mauaji ya Khashoggi, ambaye alikuwa akiandika habari katika gazeti la The Washington Post la Marekani.
Ripoti ya RSF inatoa maelezo ya matukio 34 ya Waandishi wengine wa Habari ambao wamefungwa Nchini Saudi Arabia, akiwemo Mwendesha blogu, Raif Badawi ambaye amefungwa tangu mwaka 2012 kwa makosa ya kuutukana Uislamu.