Jumla ya familia 200 za wakimbizi wa mafuriko zilifikiwa na kupokezwa misaada ya fedha, malazi, vyandarua, chakula, sabuni, dawa zikiwemo zile za kutibu maji, sodo za kusaidia wanawake na wasichana kujisitiri kipindi cha hedhi miongoni mwa misaada mingine.
Shirika la World Vision Kenya kwa ushirikiano na serikali ya kaunti ya Lamu, walifikisha misaada hiyo kwa wakimbizi hao wa mafuriko, hasa wale walioko kwenye kambi mbili kuu za Moa na Kitumbini.
Kila familia ilipokezwa jumla ya Sh10,300 kwenye mpango huo, maarufu cash transfer.
Akizungumza wakati wa shughuli ya kuwakabidhi misaada wakimbizi hao, Afisa Mkuu wa World Vision Kenya anayesimamia kaunti za Lamu, Tana River na Garissa, Michael Mulei, alisema shirika hilo litaendelea kujitahidi na kushirikiana na serikali za ugatuzi katika kuhakikisha kila mwaathiriwa wa mafuriko nchini anasaidiwa.
Mulei alitaja kuwa World Vision Kenya tayari imetafuta na kupata fedha za kima cha Sh45 milioni zitakazotumika kuwasaidia waathiriwa wa mafuriko kote nchini.
Alisema kwa ushirikiano na serikali ya kaunti ya Lamu, World Vision pia itaendeleza upokezaji wa mafunzo na elimu ya kusaidia waathiriwa kukabiliana Na changamoto zinazochangiwa na mafuriko,ikiwemo maradhi na afya kwa ujumla.
Kulingana na ripoti ya serikali ya Kaunti ya Lamu kuhusiana na janga la El-Nino, jumla ya familia 2,599 zimeathiriwa na mafuriko ambapo familia 822 zimehama makwao baada ya makazi yao kuharibiwa na mafuriko hayo.
Miongoni mwa kambi za wahanga wa mafuriko Lamu ni Moa, Kitumbini, Lumshi A na B, Mikinduni B miongoni mwa nyinginezo.