Washukiwa watano wa majasusi wa Urusi wamefikishwa katika mahakama ya Uingereza wakituhumiwa kupanga njama ya kukusanya taarifa ambazo zingefaa kwa adui.
Wanaume hao watatu na wanawake wawili, ambao wote ni Wabulgaria, walirudishwa rumande katika mahakama ya hakimu ya Westminster.
Orlin Roussev, 45, wa Great Yarmouth, Norfolk; Bizer Dzhambazov, 41, wa Harrow, kaskazini-magharibi mwa London; Katrin Ivanova, 31, wa anwani hiyo hiyo ya Harrow; Ivan Stoyanov, 31, kutoka Greenford, magharibi mwa London; na Vanya Gaberova, 29, kutoka Churchway, kaskazini magharibi mwa London, wote walionekana kwa njia ya videolink.
Wote wanashtakiwa kwa kula njama ya kukusanya taarifa zinazokusudiwa kuwa na manufaa moja kwa moja au isivyo moja kwa moja kwa adui kwa madhumuni yanayoathiri usalama na maslahi ya serikali kati ya tarehe 30 Agosti 2020 na 8 Februari mwaka huu.
Washtakiwa hao walizungumza tu ili kuthibitisha kuwa wanaweza kuona na kusikiliza mahakama na kutaja majina yao na tarehe zao za kuzaliwa wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo fupi.
Wataonekana tena huko Old Bailey tarehe 13 Oktoba.