Leo November 15, 2019 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imetoa hati ya kukamatwa wa Wabunge wanne wa CHADEMA na kufikishwa mahakamani hapo kwa kukiuka masharti ya dhamana.
Pia Mahakama, imetoa hati ya wito (Samasi) kwa wadhamini ili wafike mahakamani hapo na kujieleza kwa kwanini hawakuwapeleka washtakiwa mahakamani kama masharti ya dhamana yanavyowataka.
Wabunge hao ambao ni washtakiwa katika kesi ya uchochezi namba 112 ya mwaka 2018 ambao ni Ester Bulaya, Mbunge wa Bunda Mjini, John Heche mbunge wa Tarime Vijijini, Peter Msigwa Mbunge wa Iringa Mjini na Halima Mdee Mbunge wa Kawe.
Amri hiyo imetolewa leo na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya washtakiwa hao kutofika mahakamani wakati kesi yao ilipoitishwa kwa ajili ya kusikilizwa bila wao kuwepo na kutokuwepo kwa taarifa zozote kutoka kwao wala wadhamini wao.
Mapema kesi hiyo ilikuwa kwa ajili ya upande wa mashtaka kumuhoji mshtakiwa Mbowe baada ya kumaliza kutoa ushahidi wake wa Upande wa Utetezi lakini wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi alidai washtakiwa wengine hawapo mahakamani hivyo anaiomba mahakama kutoa hati ya washtakiwa hao kukamatwa.
Kabla ya kutoa amri hizo, Hakimu Simba amesema Novemba 15, mwaka huu kesi ilipangwa kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa leo saa 3asubuhi ndiyo sababu washtakiwa wengine waliwahi lakini hadi saa 4:05 kesi hiyo ilipoingia mahakamani, washtakiwa hao hawapo na hakuna sababu za Msingi.
Baada ya Hakimu Simba kueleza hayo, wakili wa utetezi Faraji Mangula kwa niaba ya mawakili Profesa Abdallah Safari, Peter Kibatala na Jeremiah Mtobesya aliiambia Mahakama kuwa anataarifa za Bulaya hata hivyo kabla hajaanza kueleza, Hakimu Simba alimueleza kuwa anayepaswa kuzungumza juu ya hilo ni wadhamini wa washtakiwa hao siyo Wakili.
Wakili Nchimbi ameiomba mahakama itoe hati ya kuwakamata washtakiwa hao na wito kwa wadhamini wao ili wajieleze kwa mini hawakuwapeleka washtakiwa mahakamani kama masharti ya dhamana yanavyotaka.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 19, 20 na 21, mwaka huu 2019.
Washtakiwa waliofika mahakamani leo ni Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Salum Mwalimu, Naibu katibu Mkuu bara na Mbunge wa kibamba John Mnyika, katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk Vincent Mashinji na Mbunge WA Tarime mjini Ester Matiko.
Katika Kesi hiyo Mbowe na wenzake wanaokabiliwa na mashtaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia na kuhamasisha hisia za chuki.
RAIS MAGUFULI AWA-SURPRISE MASTAA WA BONGO, APIGA SIMU LIVE KUWAUNGA MKONO