Serikali wilayani Ulanga mkoani Morogoro imewakamata watu saba akiwemo mwekezaji mzawa Junior Kasanga na raia wawili wa China kwa tuhuma za kutorosha madini ya dhahabu yenye thamani ya shilingi milioni 337.5 kutoka katika mgodi uliopo kijiji cha Isyanga wilayani humo.
Akizungumzia tukio hilo Mkuu wa wilaya ya Ulanga, Ngolo Malenya, amesema kuwa dhahabu iliyokamatwa ina uzito wa gramu 2,640 sawa na kilogramu 2.64 ambapo amebainisha serikali bado inaendelea kuwafuatilia wawekezaji wengine ambao wamekuwa na tabia ya kutorosha madini na kusababisha kupotea kwa mapato ya serikali.
Kwa upande wake Kaimu Afisa Migodi wilaya ya Ulanga, Edward Ngulinja, ameeleza awali wawekezaji hao walifika katika ofisi ya madini ya wilaya hiyo kwa ajili ya taratibu za kisheria ndipo walipo watiliashaka kuwa kuna udanganyifu wanafanya na kuvitaarifu vyombo vya ulinzi na usalama.