Wadau mbalimbali wa maendeleo nchini kutoka sekta binafsi wameombwa kushirikiana na serikali kuwekeza katika sekta ya kilimo hasa kutatua baadhi ya changamoto zinazoikumba sekta hiyo ikiwemo upatikanaji wa masoko ya uhakika ya kuuzia mazao ya Kilimo.
Wito huo umetolewa leo Agosti 23, 2024 na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Steven Muhapa ambaye pia alikuwa mgeni rasmi katika mkutano wa kutathmini miradi miwili ya Farmers Field and Business School (FFBS) na Shamba Darasa Imara na Ustadi (SADIFU PROJECT) ambayo inatekelezwa na Shirika la Care Tanzania katika Baadhi ya Wilaya za Mkoa wa Iringa na Wilaya ya Wanging’ombe Mkoani Njombe.
“Serikali ina nia njema ya kushirikiana na wadau wote kuhakikisha nguvu kubwa inawekwa katika kilimo na viwanda ili kuendelea kuondoa changamoto zinazojitokeza hasa tukizingatia masuala ya usalama wa chakula na lishe, upatikanaji wa masoko yenye tija na kuongeza kipato kwenye ngazi ya kaya ambapo serikali peke yake haiwezi kuziondoa changamoto hizi bila ninyi wadau wa sekta binafsi”, amesema Muhapa.
Malengo ya miradi hiyo ni kuongeza tija za uzalishaji, usalama wa chakula na lishe, kuongeza kipato, uhimilivu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, usawa wa kijinsia na upatikanaji wa masoko ya uhakika ya mnyororo wa thamani wa mazao ya soya na alizeti hasa kwa wakulima wanawake katika Wilaya ambazo inatekelezwa miradi hiyo.
Mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Sun Set uliopo katika Manispaa ya Iringa ukiudhuriwa na wadau mbalimbali wa kilimo kutoka katika Mkoa wa Iringa na Njombe.