Changamoto ya kutokuwa na mpango bora wa matumizi ya ardhi umeelezwa kuchangia uharibifu kwenye vyanzo vya maji kwa kusababisha muingiliano wa makazi ya watu katika vyanzo hivyo, shughuli za kibinadamu hasa kilimo na ufugaji hali inayopelekea upungufu wa Rasilimali za maji katika maeneo mengi nchini.
Kutokana na uwepo wa changamoto hiyo, Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu wamekutana wameitisha Jukwaa la Wadau wa Maji wa Sekta Mtambuka lililofanyika Mkoani Morogoro kwa lengo la kujadili kwa pamoja namna bora ya kushirikiana kuhakikisha vyanzo vya maji vinakua salama wakati wote.
Akimuwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mkurugenzi wa huduma za ubora wa maji kutoka wizara ya maji Bw. Kheri Chisute amesema jukwaa hilo litaweka mikakati na mipango kazi itakayoshughulikia changmoto zote zinazolikabili Bonde la Wami/Ruvu
Awali, Mkuu wa wilaya ya Morogoro Mhe Mussa Kilakala amekemea vikali shughuli za kibinaadamu zinazoendelea kufanywa pembezoni mwa vyanzo vya maji na kutoa wito kwa wananchi kulinda na kuhifadhi mazingira kwa mustakabali wa taifa letu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Bodi ya maji Bonde la Wami/ Ruvu Mhandisi Elibariki Mmasy ametumia Jukwaa hilo kuwaomba wadau kuendelea kushirikiana na bodi hiyo katika ulinzi madhubiti wa vyanzo hivyo ili kuepusha uvamizi katika vyanzo vya maji.
Bodi ya Maji Bonde la Wami Ruvu ilianzishwa mwaka 2002 ikihudumia mikoa 6 wilaya 27 na vijiji na mitaa 2670 huku ikichangia asilimia 3.31 ya pato la Taifa.