Wakazi wa Wilaya ya Ulanga wamepata visima vya maji vinne kutoka kwa wafadhili kutoka nchini Uswisi ambao wamekuwa wakifanya hivyo kila mwaka.
Mwakilishi wa wafadhili hao Bi Rubab Jawad Aziz amesema hatua hiyo imekuja baada ya kuona Changamoto ya maji imekuwa kubwa katika Wilaya hiyo licha ya Serikali kupambana kuitatua mara zote.
Kwa upande wao wananchi wa Wilaya ya Ulanga wamesema wanayofuraha kuona wadau wanajitokeza kuwasaidia kwani ni kweli wanapata adha kubwa ya maji hususani kipindi cha kiangazi licha ya kuwepo na miundombinu ya maji lakini haitoi maji kabisa.
Naye Mbunge wa Jimbo hilo la Ulanga Mhe Salim Alaudin Hasham amesema Changamoto ya maji katika jimbo hilo ni kubwa hivyo hawezi kuiachia Serikali pekee bali ataendelea kutafuta wadau wengi kwa lengo la kuhakikisha Changamoto hio inapungua kama sio kuisha kabisa.
Visima hivyo vinne vimechimbwa katika kata tatu ambazo ni EUGA,Chilombora, Uponera na Kichangani na tayari vinaendelea kutoa huduma za maji.
Wilaya ya Ulanga ina wananchi zaidi ya laki mbili (200000) ambao wanahitaji maji kiasi cha lita 1,600,000 lakini kwasasa wanapata lita 9000 pekee ambazo hazitoshelezi mahitaji yao.