Wafadhili katika mkutano wa Umoja wa Mataifa siku ya Jumatatu waliahidi karibu dola bilioni 1.5 kukabiliana na mzozo wa kibinadamu nchini Sudan, na kusaidia nchi ambazo ni majirani zake kuwapatia hifadhi watu wanaokimbia mapigano.
Sudan inatumbukia kwenye wimbi la maafa na uharibifu kwa kasi kubwa, mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, alionya alipokuwa akiwataka wafadhili kuingilia kati na kuzuia ongezeko la vifo kutokana na vita hivyo.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema Siku ya Jumatatu kuwa Sudan inadidimia kwenye majanga ya vifo na uharibifu mkubwa, kwa kasi ambayo haijawahi kushuhudiwa.
Umoja wa Mataifa umesema unahitaji kiasi dola bilioni 3 kufadhili shughuli zote za kibinaadamu nchini Sudan mwaka huu lakini pia kushughulikia tatizo la wakimbizi wa nchi hiyo walioko katika mataifa jirani.
Zaidi ya miezi miwili baada ya mapigano, Umoja wa Mataifa una wasiwasi kwamba mgogoro huo unaweza kusambaa na kuyumbisha mataifa jirani ya Afrika.
Mpango huu wa kukusanya msaada kwa Sudan unaratibiwa kwa pamoja na mashirika yanayohusika na masuala ya kibinadamu na wakimbizi ya Umoja wa Mataifa pamoja na Misri, Ujerumani, Qatar, Saudi Arabia, Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya