Wafanyabiashara watatu wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam wakikabiliwa na mashitaka manane likiwemo la kuisababishia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hasara ya zaidi ya Sh bilioni 1.167.
Washitakiwa hao ni Emmanuel Nkalang’ano, Rugainunula Lwekamwa na Mwita Nyakiha ambao walifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi, Joyce Mushi.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Medalakini Emmanuel akisaidiana na Jeniva Rugalama na Auni chilamula alidai kuwa washitakiwa hao wanakabiliwa na makosa ya kuhujumu uchumi ikiwemo kuongoza genge la uhalifu, kutoa risiti za uongo, kutumia kifaa cha kielektroniki kwa njia ya kupotosha mfumo, kuisababishia mamlaka husika hasara na utakatishaji fedha.
Wakili Emmanuel alidai kuwa katika mashitaka ya kwanza, katika tarehe tofauti kati ya Agosti 2022 na Agosti 2023 eneo la Kariakoo Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam washitakiwa wote kwa pamoja walipanga njama za uhalifu kwa kutoa risiti za uongo kwa nia ya kujipatia faida.
Alidai kuwa katika tarehe tofauti kati ya Agosti 2022 na Desemba 2022 eneo la Kariakoo Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam, kwa pamoja walitoa risiti za uongo kutoka kampuni ya Vartual Fiscal Device iliyosajiliwa kwa jina la Rugainunula kwa nia ya kumdanganya Kamishna kuwalipa walipakodi wengine Kodi ya Ongezeko la Thamani ya Sh 150,987,915.31/-
Pia, inadaiwa kuwa, Nkalang’ano, Rugainunula na Nyakiha kwa tarehe tofauti kati ya Januari 2023 na Agosti 2023 eneo la Kariakoo Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam, kwa pamoja walitoa risiti za uongo kutoka kwa Kampuni ya Vartual Fiscal Device iliyosajiliwa kwa jina la Rugainunula kwa nia ya kumlaghai Kamishna ili kuwalipa walipa kodi wengine Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) 1,167,537,867.58/-
Katika mashitaka ya kutumia vifaa vya kielektroniki kwa njia ya kupotosha mfumo, inadaiwa washitakiwa wote kati ya Agosti 2022 na Desemba 2022 eneo la Kariakoo Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam, walitumia Vartual Fiscal Device iliyosajiiwa kwa jina la Rugainunula kutoa risiti za uongo za fedha zilizopakiwa katika mfumo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania ili kuwaongezea walipa kodi ili kudai marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ya Tsh 150,987,915.31/-
Pia alidai kuwa kati ya Januari 2023 na Agosti 2023 katika eneo hilo hilo, washitakiwa wote kwa pamoja walitumia Vartual Fiscal Device iliyosajiliwa kwa jina la Rugainunula kutoa risiti za uongo zilizopakiwa katika mfumo wa TRA hivyo kusababisha walipa kodi wengine kudai marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ya Sh bilioni 1.16/-
Katika mashitaka ya kuisababishia hasara mamlaka hiyo, washitakiwa wote wanaodaiwa kwa tarehe tofauti kati ya Agosti 2022 na Desemba 2022 kwa makusudi waliisababishia TRA hasara ya Sh 150,987,915.31/-.
Pia, inadaiwa kuwa kwa kitendo hicho, waliisababishia TRA hasara ya Sh bilioni 1.167.
Wakili Emmanuel alidai katika tarehe tofauti kati ya Agosti 2022 na Desemba 2022 katika eneo la Kariakoo Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, washitakiwa wote walifanya muamala wa fedha kiasi cha Sh 150,987,915.31 huku wakijua kuwa fedha hizo ni zao la uhalifu.
Inadaiwa washtakiwa wote kwa pamoja pia, walijihusisha na muamala wa Sh bilioni 1.167 huku wakijua kuwa fedha hizo ni mapato ya kosa la awali la kuongoza genge la uhalifu wa kupangwa.
Hakimu Mushi, aliwataka washitakiwa kutojibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi na kwamba haina mamlaka ya kutoa dhamana kwa sababu mashitaka ya utakatishaji fedha hayana dhamana.
Hakimu huyo aliahiriaha kesi hiyo hadi Desemba 28, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.