Rais wa Kituo cha Uwekezaji na Maendeleo cha Waarabu na Afrika (Arab-African Centre for Investment and Development-CAAID), Dkt. Amine Boutalbi amesema kuwa CAAID inaratibu ushiriki wa wafanyabiashara wa Algeria katika maonesho ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) maarufu Maonesho ya Saba Saba kwa mwaka 2024.
Dkt. Boutalbi amesema hayo wakati alipokutana kwa mazungumzo na Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Iman Njalikai katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania Jijini Algiers tarehe 26 Oktoba 2023.
Aidha, Dkt. Amine Boutalbi ameahidi kuwa CAAID itashirikiana na Ubalozi wa Tanzania nchini Algeria kuratibu kongamano maalum la wafanyabishara wa Algeria litakalofanyika nchini Tanzania mwaka 2024 kwa lengo la kuimarisha uwekezaji na biashara kati ya wafanyabiashara wa nchi hizi mbili.
Kwa upande wake, Balozi Njalikai ameahidi kuwa atashirikiana na kituo hicho ambacho ni kiungo muhimu kati ya Ubalozi na Sekta Binafsi nchini Algeria.
Mhe. Balozi amehidi pia ofisi yake itashirikiana na mamlaka za Tanzania hususan TPSF, TIC na TANTRADE ili kufanikisha ushiriki wa wafanyabiashara wa Tanzania kwenye makongamano ya uwekezaji na biashara yanayoandaliwa na Kituo cha CAAID mwezi Mei 2024