Wafanyabiashara wa Madini nchini wametakiwa kurejesha nchini fedha za kigeni zinazotokana na mauzo ya madini nje ya nchi ili zisaidie kuimarisha uchumi wa nchi.
Kauli ya Serikali imetolewa na Waziri wa Madini Dkt.Dotto Biteko wakati wa kikao chake na Wafanyabiashara hao jijini Dodoma kutoka nchi kilichohudhuriwa na Viongozi waandamizi wa Wizara hiyo na Taasisi zake, Mwakilishi kutoka Benki Kuu ya Tanzania na Maafisa Madini Wakazi kutoka mikoa mbalimbali nchini.
Waziri Dkt. Biteko amesema kwa mujibu wa kifungu cha 5.1 cha Sera ya madini kinasisitiza Ustawi wa masuala ya kiuchumi ikiwemo ustawi wa huduma za benki nchini ili kuleta manufaa kwa Serikali na sekta binafsi.
Kutokana na kifungu hicho Dkt. Biteko amesema “wizara ingependa kuona fedha za mauzo ya madini zinarejeshwa nchini kama Sheria inavyoelekeza kupitia mifumo ya kibenki na kwa kuzingatia sheria zote za nchi na kuongeza kwamba, hayo yote yanalenga kuboresha shughuli za Madini nchini kutokana na umuhimu wa Sekta hiyo kiuchumi”.
Aidha, Dkt.Biteko ametambua mchango wa wafanyabiashara hao kupitia Masoko ya Madini nchini na kusema katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2022/23 Julai 2022 hadi Juni 2023, waliweza kuuza madini nje ya nchi yenye thamani ya Shilingi trilioni 2.24.
‘’Katika kipindi hicho, Serikali ilikusanya kiasi cha Shilingi bilioni 157.44 kama malipo ya mrabaha na ada ya ukaguzi, sawa na asilimia 25 ya mrabaha uliokusanywa kwa madini yote. Nachukua fursa hii kuwapongeza kwa mchango wenu huo,’’ amesema Dkt. Biteko.