Wafugaji na wafanyabiashara wa nguruwe na mazao yake wanaofanya shughuli zao Wilayani Kahama, Mkoani Shinyanga wameiomba Serikali kuendelea kuchukua hatua za haraka kuudhibiti mlipuko wa ugonjwa wa Homa ya Nguruwe ulioikumba wilaya hiyo na kuathiri kwa kiasi kikubwa shughuli zao za kiuchumi.
Wafugaji na wafanyabiashara hao walitoa ombi hilo Januari 26, 2021 wakati walipokuwa wakiongea na Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Hezron Nonga alipokwenda Wilayani Kahama kwa ajili ya kuongeza nguvu kwa timu iliyoundwa na Serikali ya kudhibiti ugonjwa huo.
Wakiongea kwa nyakati tofauti, wafugaji na Wafanyabiashara hao walisema kuwa tangu ugonjwa huo uingie katika wilaya ya Kahama umesababisha hasara kubwa kwa wafugaji na wafanyabiashara kwa sababu nguruwe wengi wamekufa huku biashara ya mazao ya nguruwe hususan uuzaji wa nyama ukizorota kwa kiasi kikubwa.
Wilson Sawa, Mmiliki wa Baa na Muuza nyama ya nguruwe wilayani Kahama alisema kuwa biashara ya nyama ya nguruwe imekuwa ikisaidia biashara nyingine lakini tangu kusitishwa kwa biashara hiyo baa nyingi ambazo zinauza nyama ya nguruwe hazifanyi vizuri.
“Kusitishwa kwa biashara hii kumeathiri uchumi wetu kwa sehemu kubwa, tunaiomba serikali iharakishe kuudhibiti ugonjwa huu na iendelee kufanya tathimini ya maendeleo ya ugonjwa ili kama unapungua waturuhusu tuendelee kufanya biashara,” Sawa.
Naye, Pendo Emmanuel, mmliki wa bucha ya nyama ya nguruwe katika wilaya hiyo alisema kabla ya ugonjwa huo kwa siku alikuwa anauza hadi kilo 80 kwa bei ya jumla na rejareja lakini kwa sasa baada ya ugonjwa hakuna biashara anayoifanya.
“Kwa kweli ugonjwa huu umeathiri kwa kiwango kikubwa katika kuendesha Maisha yangu, siwezi kupeleka watoto shuleni, tunaiomba Serikali ione itakavyoweza kutusaidia ili tuweze kuendesha maisha yetu,” Emmanuel.
Frank Kimaro, Mfugaji wa Nguruwe, Wilayani Kahama alisema kuwa kutokuwepo na sehemu rasmi ya kuchinjia Nguruwe kumechangia kwa namna moja au nyingine katika kusambaza ugonjwa huo kwa sababu wakati wote wamekuwa wakichinja nguruwe wao katika maeneo yalipo mabanda yao.
“Ombi langu kwa Serikali ituwekee sehemu itakayokuwa maalum kwa ajili ya kuchinja nguruwe wetu hii itasaidia kudhibiti milipuko ya magonjwa lakini Serikali nayo itapata mapato yake,” Kimaro
Akizungumza kuhusu hali halisi ya kuenea kwa ugonjwa huo wa homa ya nguruwe, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji, Kahama, Anderson Msumba alisema kuwa Serikali ipo kazini kuhakikisha ugonjwa huo unadhibitiwa haraka ili shughuli za ufugaji na biashara ya nguruwe na mazao yake ziweze kuendelea kama kawaida.
Aliongeza kwa kusema kuwa tangu Serikali ilipoingilia kati sakata la ugonjwa huo kwa kupeleka timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuungana na wataalam wa Halmashauri idadi ya vifo imeanza kupungua na anaamini kwa juhudu zinazoendelea ugonjwa huo sio muda mrefu utakoma.
“Nitoe wito kwa wafugaji kuendelea kutoa ushirikiano kwa timu ya wataalam ambayo imewekwa na Serikali kwa ajili ya kusaidia kutokomeza ugonjwa huo ikiwemo kuhakikisha mifugo yao haitoki nje ya mabanda yao, na wasiwe na tamaa, waache kuchinja nguruwe wagonjwa kwa sababu atakayebainika hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake,” Msumba.
Aidha, Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Hezron Nonga pamoja na kutoa elimu ya kina kuhusu hatua za kuchukua katika kudhibiti ugonjwa huo usisambae, pia aliwataka wafugaji na wale wote wanaojihusisha na biashara ya nguruwe kuzingatia masharti ya karantini iliyowekwa na Serikali na atakayekaidi agizo hilo la Serikali sheria itachukua mkondo wake.
Amesema kuwa Sheria ya Magonjwa ya Wanyama Na. 17 ya Mwaka 2003 inazuia shughuli za uchinjaji na usambazaji wa mifugo na mazao yake katika maeneo yenye mlipuko wa magonjwa, na yeyote atakayekwenda kinyume na Sheria hiyo akibainika atapewa adhabu ya papo kwa papo ya faini ya shilingi milioni tano (5) au akipelekwa Mahakamani na kupatikana na hatia atahukumiwa adhabu yake ni kulipa faini ya shilingi milioni kumi (10) au kifungo cha mwaka mmoja jela au vyote kwa pamoja.