Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, TAMISEMI anayeshughulikia Afya, Dkt. Wilson Mahera amewataka waganga wafawidhi wa vituo vya kutolea huduma za afya ngazi ya msingi kuhakikisha wanawekeza katika mafunzo ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia na kutoa huduma bora za afya kwa watanzania.
Akizungumza wakati wa kufungua mkutano wa Waganga Wafawidhi wa vituo vya kutolea huduma za afya ngazi ya Msingi, Dkt. Mahera amesema waganga wafawidhi wanapaswa kuwekeza katika mafunzo kwa ajili ya maendeleo ya kitaalamu.
“Waganga wafawidhi wanapaswa kuwekeza katika mafunzo kwa ajili ya maendeleo ya kitaaluma ili kuhakikisha wanapata uelewa mpya na kuweza kwendana na mabadiliko ya teknolojia katika sekta ya afya, mkifanya hivyo kutawawezesha wanaweza kutoa huduma bora na hasa za kisasa kwa jamii ya kitanzania katika maeneo yenu,”amesema.
Pia ametoa wito kwa waganga wafawidhi hao kila mmoja wao kujitoa kikamilifu katika kutekeleza majukumu na kuwa karibu na jamii wanayoihudumia.
Akizungumzia mkutano huo, Dkt. Mahera amesema mada kadhaa zimewasilishwa ikiwa ni pamoja na utekelezaji na uboreshaji huduma za afya, utawi wa jamii na lishe, hali ya huduma katika vituo vya kutolewa huzuma za afya, hali ya utekelezaji na ufuatiliaji wa ujenzi na ukarabati wa miradi ya mbalimbali ikiwemo ya miundombinu.
“Kupitia mkutano huyo tumeweza kubaini kuwa kwenye vituo vyetu vya kutolea huduma za afya na hospitali za wilaya kuna upungufu na uhitaji mkubwa wa maafisa ustawi wa jamii,”amesema.