WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema wagombea wa urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) hawatakuwa na kazi kubwa kwa kuwa wataingia katika uchaguzi wakiwa na rekodi thabiti ya utekelezaji ilani ya chama.
Akizungumza katika mkutano wa CCM Jimbo la Maswa, mkoani Simiyu jana, Majaliwa alisema kuwa katika kipindi cha kuelekea kwenye uchaguzi, chama hicho kitaendelea kuwaeleza wananchi mafanikio yaliyopatikana.
Alisema suala hilo litafanyika kimkakati ili wagombea wa chama hicho kwa ngazi ya urais na wabunge wasiwe na kazi kubwa ya kueleza waliyoyafanya, badala yake wakipita majimboni watumie muda wao kuomba kura.
“CCM ni chama kikubwa, kinachopendwa na kinachoaminiwa, kina sera zinazotekelezeka, kikiahidi kinatekeleza. Wanamaswa, leo mpo hapa na mbunge wa Maswa Mashariki, anawaeleza yanayotekelezwa ili mgombea wetu atakapofika hapa, kazi yake iwe ni ndogo ya kuomba kura,” alisema.
Majaliwa alieleza kuwa wakati wa kampeni, Mgombea Urais kupitia CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan pamoja na mgombea mwenza wake, Dk. Emmanuel Nchimbi watafika Maswa kuzungumza na wananchi na kueleza mipango na mikakati yao kwa miaka mitano ijayo.
“Wakati wa kampeni, Rais Samia na mgombea mwenza wake Dk. Nchimbi watakuja Maswa kuomba ridhaa yenu. Tunataka kazi yao iwe nyepesi kwa sababu tayari mmeona kazi nzuri iliyotekelezwa hasa katika kusogezea wananchi huduma kwa kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo,” alisema Majaliwa.