Rais Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania ina zaidi ya wagonjwa 100 wa Covid-19 na kuwataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari ili idadi hiyo isiongezeke zaidi.
Ameeleza hayo Ikulu jijini Dar es Salaam wakati akijibu maswali mbalimbali yaliyoulizwa na wahariri wa vyombo vya habari katika mkutano huo wa tathmini ya siku 100 tangu awe kiongozi mkuu wa nchi.
Amesema ugonjwa huo upo Tanzania na kuna wagonjwa wanaendelea kupata matibabu, wengi wanatibiwa kwa kutumia gesi kutokana na hali zao kuwa mbaya zaidi.
“Nataka niwe mkweli, Tanzania tuna wagonjwa katika hili wimbi la tatu. Mpaka taarifa nilizozipata juzi, nadhani kuna wagonjwa kama 100 na…, kati yao si chini ya 70 wako kwenye matibabu ya gesi, wengine wako kwenye matibabu ya kawaida,” Rais Samia.
Amesema ukiangalia idadi yao si kubwa lakini hawana budi kujikinga ili wasiongezeke na kwamba Serikali imechukua hatua ya kuchanja na chanjo hiyo itakuwa ya hiari kwa watu ambao watapenda kufanya hivyo.
“Watanzania wengine wameshakwenda kuchanja wapo waliokwenda Dubai, Afrika Kusini…, kwa hiyo tukasema chanjo zije ili watu wachanje kwa hiari,” Rais Samia.