Idara ya Uhamiaji Mkoani Iringa kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa limefanikiwa kuwakamata wahamiaji haramu raia wa Ethiopia 16 jinsia ya kiume kwa kosa la kuingia nchini kinyume cha sheria mnamo tarehe 06 Aprili 2024 katika maeneo ya msitu wa Luganga kata ya SaoHill Tarafa ya Ifwagi Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa waliotelekezwa kwenye shamba la mahindi.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari Jana tarehe 08 Aprili 2024 katika Mji wa Mafinga Afisa Uhamiaji Mkoa wa Iringa Kamishna Msaidizi (ACI) Peter Kimario alisema uchunguzi wa awali ulibaini kua raia hao wa kigeni walishushwa kwenye gari awali ilisomeka STL 3999 aina ya Landcruser V8 VXR rangi nyeupe ambayo dereva wake aliitelekeza na kutokomea kusikojulikana, baada ya uchunguzi wa awali kati ya Idara ya uhamiaji na Jeshi la Polisi umebaini gari hiyo imesajiliwa kwa namba T.803 CVW yenye chasisi namba URJ 202-5001217 na injini namba 1UR-FE
Idara ya Uhamiaji inaendelea na taratibu za kuwafikisha mahakamani watuhumiwa hao kwa kosa la kuingia nchini kinyume cha sheria.
ACI Kimario ametoa rai kwa wananchi Mkoani humo kuendeleza Ushirikiano na vyombo vya Ulinzi na Usalama katika Masuala ya Ulinzi na Usalama sanjari na kuendelea kushiriki katika kampeni ya Uhamiaji ya “MJUE JIRANI YAKO” inayoendelea nchini.
Aidha amewaomba wanachi hao kuacha kuishi kienyeji na watu wasiojulikana au mtu yoyote atakaetiliwa shaka kwani raia yoyote wa kigeni anapoingia nchini kinyume na sheria ni vigumu kujua anangia kwa lengo gani hivyo ni muhimu kutoa taarifa mapema kwa Idara ya uhamiaji na vyombo vingine vya ulinzi na usalama Ili kuhakikisha Nchi inaendelea kubaki salama
Bukumbi amesema wahamiaji hao bado wanashikiliwa na jeshi la polisi kwa uchunguzi na upelelezi zaidi na baadae watafikishwa mahakamani.