Mkuu wa Wilaya ya Babati Mhe. Emmanuela Mtatifikolo Kaganda amewataka washiriki waliohitimu mafunzo ya Jeshi la Akiba kuwa chachu ya Mabadiliko katika jamii kwa kujitunza na kuwa wazalendo wa Taifa pamoja na Amani ya nchi.
Mhe. Kaganda ametoa maelekezo hayo leo Novemba 22, 2024 wakati akifunga mafunzo ya Jeshi la Akiba Tarafa ya Mbugwe Kata ya Mwada uwanja wa CCM ikiwa wahitimu zaidi ya 370 wamehitimisha mafunzo hayo.
Aidha, Mhe. Kaganda amewataka waliohitimu mafunzo hayo kuwa mabalozi kwa vijana wengine katika jamii huku akisisitiza wazazi kuendelea kuwapa moyo vijana ili kuendelea kushiriki katika Mafunzo ya Jeshi la akiba yanapoitishwa katika mitaa mbalimbali.
Kufuatia mafunzo waliyopokea Mhe. Kaganda amewataka wahitimu hao kutumia vizuri mafunzo hayo katika kujilinda na kulinda taifa kwa ujumla na kuweka angalizo kutokuyatumia mafunzo hayo tofauti na yale waliyofundishwa
“Vijana mliopata mafunzo na kuhitimishwa siku ya Leo mtakwenda kuwa walinzi wazuri wa jamii yetu, Wilaya yetu na Taifa kwa ujumla” amesema Mhe. Kaganda
Kwa upande wake Mshauri wa Jeshi la Akiba kwa Wilaya ya Babati Afande Machupa amesema mafunzo hayo yalianza rasmi tarehe 18 Juni, 2024 ikiwa na idadi ya wanafunzi 150 lakini kutokana na jitihada za viongozi wa Kata idadi hiyo iliongezeka hadi kufikia 408 ikiwemo wanaume 362 na wanawake 46.
Katika hatua nyingine Afande Machupa amekiri kuwa idadi hiyo ya wanafunzi wengi hasa kwa upande wa wanawake kuwa “imevunja rekodi” huku akitaja malengo ya mafunzo hayo ni pamoja na kumwezesha mwananchi kuweza kulinda taifa lake katika hali mbalimbali ikiwa ni pamoja na kumwezesha kufanya kazi za usalamawa raia wakati wa Amani na kushiriki vita wakati wa Hatari.
Kwa upande wao wahitimu wamekiri kupokea mafunzo mbalimbali kupitia jeshi hilo huku wakipatiwa mafunzo ya vitu mbalimbali kama huduma ya kwanza, elimu ya TAKUKURU, ujasiriamali na mafunzo mengine yatakayowasaidia pindi watakaporejea uraiani.