Baadhi ya Waislamu Nchini Burundi wameendelea kupaza sauti za kutaka kuachiwa huru kwa Sheikh Rashidi Ndikumana aliyekamatwa na Polisi baada ya kumtaka Waziri wa Mambo ya Ndani wa Burundi kuwaomba radhi Waislamu kufuatia tamko lake hivi karibuni.
Hii ni baada ya Waziri huyo aitwae Gervais Ndirakobuca kuongea kwenye mkutano na Viongozi wa dini mbalimbali Burundi na kusema Wananchi wanakerwa na kelele za Makanisa na Adhana za Misikiti na kusema adhana alfajiri ni kero kwa Raia kwani ni jukumu lao Waumini kujua wakati wa kusali bila kukumbushwa na adhana.
Baada ya matamshi hayo kulizuka vuta nikuvute kati ya Polisi na baadhi ya Waumini katika mtaa wa Buterere kusini mwa Bujumbura ambako Sheikh huyo anaishi na kuongoza Masjid Madina ambapo Sheikh huyo alimtaka Waziri huyo kutambua kwamba adhana katika Uislamu ilikuwepo kabla ya kuzaliwa kwake na itaendelea kuwepo na akamuagiza kuwataka radhi Waislam katika kipindi kisichozidi wiki moja lasivyo watamuomba Rais Evariste Ndayishimiye kumfuta kazi.