Wakala wa kiungo wa Chelsea Enzo Fernandez amekanusha ripoti kwamba mchezaji huyo anajuta kusaini mkataba wa miaka minane na klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Uingereza.
Fernandez alihamia Chelsea kutoka Benfica mwaka mmoja uliopita kwa mkataba wa thamani ya £107m. Alikabidhiwa mkataba hadi 2031 ili kueneza gharama ya kandarasi yake kwa muda mrefu chini ya sheria za faida na uendelevu.
Ripoti za gazeti la The Athletic mapema wiki hii zilisema baadhi ya wachezaji hawakuwa na furaha na hawakupenda mwelekeo ambao klabu ilikuwa inaenda, ingawa hakuna watu waliotajwa.
“Mchezaji hana nia ya kuondoka,” Uriel Perez aliiambia Diario AS. “Uongozi wa Chelsea ulikuwa wazi sana na mradi huu.
“Ni mpango ambao siku zote ulikuwa mgumu mwanzoni kwa sababu wachezaji wapya na wachanga wangekuja. Lakini wakati vipande vya timu vikiwa sawa, Chelsea itasonga mbele.
“Hamu ya Enzo ni kuwa kwenye timu na kushinda mataji. Hatujakutana na klabu yoyote au hata kujaribu kuzungumza na klabu yoyote, hiyo si kweli.
“Tunajua matakwa ya mchezaji huyo ni nini. Ni wazi angependa Chelsea iwe katika nafasi nzuri zaidi [katika ligi] lakini hilo litafikiwa kwa bidii.”
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 alifunga bao Jumatano usiku wakati Chelsea ikishinda 3-1 dhidi ya Aston Villa katika mechi ya marudiano ya raundi ya nne ya Kombe la FA.