Wakandarasi wanaotekeleza miradi mbalimbali ya Kimkakati ya Nishati hususani miradi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wametakiwa kufanya kazi kwa uadilifu na kukamilisha kwa wakati na REA kuwasimamia wakandarasi kwa kutenda haki.
Hayo yamebainishwa leo Agosti 20, 2024 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko wakati wa hafla ya Utiaji Saini Mikataba ya utekelezaji wa Miradi wa Kupeleka Umeme katika vitongoji 3,060 (15 kila Jimbo) jijini Dodoma.
“Zipo taarifa za wakandarasi wanawaomba fedha wananchi wanapopeleka umeme vijijini ilhali Serikali imekwisha walipa, Nawaomba REA na Wakandarasi, nikiletewa taarifa yoyote nitachukua hatua, tendeni haki kwa wote, ” Amesema Dkt. Biteko.
Vile vile, Serikali imedhamiria kufikisha umeme katika vitongoji vyote chini ili kuongeza hali ya upatikanaji wa umeme pamoja na uunganishwaji katika maeneo ya vijijini.
Ameongeza kuwa, mpango wa kupeleka umeme kwenye vitongoji utatekelezwa kwa awamu ambapo, leo tumeshuhudia vitongoji takribani 3,060 vitapatiwa umeme kupitia mradi huu kwa gharama ya Jumla ya bilioni 366.
Pia, kwa takribani miaka 17 hadi sasa, Serikali imekuwa ikishirikiana na Washirika wa maendeleo katika utekelezaji miradi mbalimbali ya kimkakati ya Nishati bora vijijini.
“Mikataba hii tuliyoishudia leo yenye thamani ya Shilingi 362,825,108,211.45 imewezeshwa kupitia ushirikiano baina ya Serikali na Benki ya Dunia. Hivyo, kwa niaba ya Serikali ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, naomba niwashukuru Washirika wa Maendeleo wanaochangia katika mfuko wetu wa Nishati Vijijini hususan Benki ya Dunia, Serikali za Norway na Sweden, Umoja wa Nchi za Ulaya (EU), Shirika la Fedha Duniani (IMF), Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD),” amesema Dkt. Biteko.
“Wananchi wanaotarajia kunufaika na mradi huu wanayo matarajio makubwa kuwa upatikanaji wa nishati ya Umeme utaboresha na kuinua hali zao za maisha kupitia ushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi. Niwahakikishie Wananchi wote kuwa Serikali itaendelea kutenga fedha, na kushirikiana na wabia wa maendeleo kuhakikisha kuwa umeme unawafikia Watanzania wote, popote walipo, ” ameongeza Dkt. Biteko.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Mhe. David Mathayo David ameipongeza Serikali kwa hatua ya kupeleka umeme kwenye vitongoji 3,060 jambo ambalo linakwenda kutekelezwa sasa na REA.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Hassan Said, amesema matarajio yaliyopo sasa ifikapo mwezi Septemba 2024 ni kuhakikisha wanakamilisha upelekaji wa umeme kwa vijiji vyote hapa nchini.