Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameuagiza Wakala wa Barabara nchini TANROADS, kuanzia sasa kutowapa kazi Wakandarasi wote wanaochelewesha miradi ya ujenzi na menejimenti zao kuhakikisha wanaripoti ofisini kwake mara moja kwa hatua zaidi.
Amewataka Wasimamizi wa miradi ya barabara kuwa wabunifu na kusimamia majukumu yao kikamilifu ili kuondoa changamoto kwa watumiaji wa miundombinu ya ujenzi wa barabara nchini.
Bashungwa amesema hayo jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya kukagua athari za mvua, mradi wa mabasi yaendayo kasi awamu ya tatu na miradi mingine ya ujenzi inayoendelea .
Amewaagiza Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kuanzia sasa mradi wowote wa barabara unaojengwa nchini katika hatua ya usanifu lazima washirikiane na taasisi zingine za Serikali ili kuondoa matatizo ya kiutendaji pale ambapo mradi unakamilika na taasisi nyingine inataka kutekeleza mradi wake eneo hilo.
Amesema atakuwa mkali kwa watendaji au Wakandarasi wazembe wanaoshindwa kwenda na kasi ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kusababisha miradi kusuasua.
Bashungwa ameonya tabia ya baadhi ya wakandarasi kujujilimbikizia miradi mingi kwa wakati mmoja na yote kutotekelezwa kwa kasi inayotakiwa kimkataba.
“Serikali inapotoa fedha inahitaji huduma kwa haraka hivyo Mameneja nchini kote hakikisheni miradi inakamilika kwa wakati”, amesisitiza Waziri Bashungwa
Aidha, Ametoa wito kwa wakandarasi wazawa kufanya kazi kwa bidii ili kuleta tija na kuliwezesha Serikali kuwaamini na kuwapa miradi mingi ili kukuza uchumi wa watanzania.
Nae, Kaimu mtendaji Mkuu wa TANROADS, Eng. Dorothy Mtenga amesema ujenzi wa BRT III unaotekelezwa na mkandarasi Sinohydro unatarajia kukamilila Machi 2024.