Mashambulizi mabaya ya mpakani kati ya wanamgambo Lebanon Hezbollah na jeshi la Israel yameongezeka, na wakazi wa kusini mwa Lebanon wanakimbia makwao, wakihofia kuwa ghasia zinaweza kuongezeka zaidi.
Shirika la Kimataifa la Uhamiaji linakadiria kuwa karibu watu 20,000 wamekimbia makazi yao tangu vita vya Israel na Hamas vilipozuka, tarehe 7 Oktoba, wengi wao kutoka maeneo ya kusini mwa nchi.
Tumekuwa katika vijiji vilivyo kwenye mpaka katika siku za hivi karibuni, na nyingi hazina watu, maduka yamefungwa na mitaa ikiwa imeachwa.
Katika jiji la kusini la Tiro, mamia ya watu, bila mahali pa kwenda, wamepata hifadhi katika shule za umma ambazo zimegeuzwa kuwa makao.
Ijapokuwa mashambulizi ya mpakani yameshika kasi, vurugu hizo hadi sasa zimedhibitiwa.
Lakini wengi hapa bado wanakumbuka uharibifu ulioletwa na vita vya mwezi mzima kati ya Israeli na Hezbollah, na wanaogopa kwamba historia inaweza kujirudia.