Wakili wa ngazi ya juu wa Uingereza amechaguliwa kuwa mwenesha mashitaka Mkuu ajaye wa mahakama ya kimataifa ya jinai (ICC).
Karim Khan, mwenye umri wa miaka 50,kwa sasa anaongoza uchunguzi wa Umoja wa Mataifa juu ya uhalifu wa kivita uliotekelezwa na kikundi cha Islamic State nchini Iraq.
Mwandishi wa BBC wa masuala ya diplomasia James Landale amesema kuwa mafanikio katika uchaguzi uliokuwa na mpambano mkali unaweza kuangaliwa kama ushindi wa kiplomasia kwa Uingereza baada ya kujiondoa katika Muungano wa EU.
ICC ndio taasisi pekee ya kudumu inayochunguza uhalifu dhidi ya binadamu.
Bw Khan amepata ushindi wa kura 72 kati ya 123 za nchi wanachama katika awamu ya pili ya uchaguzi, na ataanza muhula wake wa miaka tisa katika mahakama hiyo mjini the Hague mwezi Juni.
Amewashinda wagombea kutoka Ireland, Italia na Uhispania.