Wakulima wa Mkoa wa Mtwara leo August 11,2023 wamekubali kuuza mbaazi zao kwa bei ya juu ya Tsh. 2003 na bei ya chini Tsh. 1,950 katika mnada wa kwanza wa zao la mbaazi ambao umefanyika kwa mara ya kwanza kwa mfumo wa stakabadhi ghalani.
Wakulima hao wameuza mbaazi hizo kupitia Chama Kikuu cha Ushirika wa Wilaya za Masasi, Mtwara na Nanyumbu (MAMCU LTD) ambapo Meneja Mkuu wa MAMCU LTD Biadia Matipa ameipongeza Serikali kwa kuingiza zao la mbaazi katika mfumo wa stakabadhi ghalani na kusema ni kwa mara ya kwanza Chama hicho kufanya mnada wa mbaazi kwa kutumia mfumo wa stakabadhi ya mazao ghalani.
Mnada huo umefanyika katika Kijiji cha Mkululu Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara na kwamba bei zilizouzwa Mbaazi hizo zinaashiria mwanzo nzuri.
“Kwa mara ya kwanza MAMCU LTD tumefanya mnada wa Mbaazi na tunashukuru Mungu wakulima wameipokea vizuri bei ya mbaazi, ila tunatoa wito kwa Wakulima kuepuka kuuza mbaazi kwa wanunuzi holela kwa magendo (kangomba) bali wapeleke kwenye vyama vya msingi ili kuepuka kudhulumiwa bei”
Nao baadhi ya wakulima katika mnada huo wameipongeza serikali kwa bei nzuri waliyoitangaza huku wakitoa wito Kwa wanunuzi kuongeza bei zaidi ili waweze kujikwamua kiuchumi, kwa muda mrefu wakulima wa zao la Mbaazi wamekuwa katika wakati mgumu kwa kukosa soko lazao hilo na bei nzuri, na hatimaye MAMCU LTD wamekuwa wakombozi Kwa wakulima.