Wakulima wa Vyama vya Ushirika nchini wamepewa wito wa kuboresha maisha yao kwa kuweka akiba baada ya msimu wa mavuno ya mazao yao ili akiba hizo ziwasaidie hususan wanapopata changamoto mbalimbali za kimaisha na kwamba hiyo itawasaidia kumudu maisha hata yanapotokea magonjwa ya mlipuko kama corona.
Wito huo umetolewa na Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) Dkt. Benson Ndiege wakati alipotembelea Chama cha Ushirika wa Wakulima wadogo wadogo wa Kilimo cha umwagiliaji Mpunga Dakawa (UWAWAKUDA LTD) kwenye ziara ya Kikazi, Mkoani Morogoro.
Mrajis amesema kuwa wanachama wa Ushirika wanaweza kutumia fursa ya kuwa pamoja katika Chama kwa kuimarisha Ushirika wao kwa kujiwekea utaratibu maalum wa kutunza akiba zinazotokana na mauzo ya mazao pale wanapovuna, na kusema kuwa utaratibu huo utakaposimamiwa vizuri kwa taratibu za kiushirika unaweza kuongeza fursa nyingine ya kuwa na Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo.
“Kila mkulima anapovuna anaweza kujiwekea akiba katika mfuko wao ambao utatumiwa na Wanaushirika kwa mahitaji yao mbalimbali pamoja na dharura zinapojitokeza kwa mwanachama”-Mrajis