Serikali imewataka wakurugenzi wa halmashauri nchini kuhakikisha wanatenga fedha kwa ajili ya sekta ya ardhi katika kipindi hiki cha maandalizi ya bajeti ya mwaka 2024/2025 kwa yale maeneo yasiyotengewa fedha za mradi wa uboreshaji usalama wa milki za ardhi nchini.
Hayo yamebainishwa tarehe 28 Novemba 2023 na Waziri Mkuu Mhe. Kasim Majaliwa katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa wakati wa Mkutano wa Kitaifa wa Wadau Kujadili Utekelezaji Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi uliofanyika jijini Dodoma.
Kupitia hotuba yake hiyo, Mhe. Majaliwa amewataka wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa halmashauri zote nchini zinazotekeleza mradi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa timu zinazotekela mradi katika maeneo yao.
‘’Ili mradi ufanikiwe ni vyema wadau wakashiriki kikamilifu katika mradi na nieendelee kuhimiza wakuu wa mikoa na wilaya pamoja na wakurugenzi wa halmashauri kutoa ushirikiano kwa timu za utekelezaji mradi’’ alisema Majaliwa
Aidha, amezitaka Taasisi zinazofanya kazi na mradi kama vile NIDA, NEMC, Tume ya Matumizi ya Mipango Bora ya Ardhi na taasisi zote kutoa ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza mradi wa uboreshaji usalama wa milki za ardhi.
Amewataka wataalamu wa sekta ya ardhi kuhakikisha pia wanashirikiana na na viongozi wa serikali za mitaa na vijiji katika kuwapa wananchi elimu kuhusu masuala ya ardhi hususan zile taarifa za utekelezaji mradi.