Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri za Longido, Same, Uvinza na Bumbuli kujitathmini kama wanatosha kuendelea kuwa katika nafasi hizo.
Waziri Ummy ameyasema hayo wakati akitoa taarifa ya Ukusanyaji wa Mapato ya ndani ya Halmashauri katika kipindi cha Julai 2020 hadi Machi 2021 mapema leo Jijini Dodoma.
Amesema Wakurugenzi wa Halmashauri zilizokusanya mapato chini ya asilimia 75 wanatakiwa kujitathmini na hawa wa Halmashauri 4 wanatakiwa kujitathimini zaidi.
“Mkurugenzi wa Halmashauri ya Longido kwa mara ya pili sasa anaingiza fedha ambazo si za mapato ya ndani kwenye mfumo wamapato ili ionekane wamekusanya zaidi; Mara ya kwanza tungeweza kuvumilia lakini kwa mara ya pili sasa ameingiza fedha walizolipwa Fidia kutoa Wakala wa Umeme vijijini (REA) kwenye mfumo wa mapato takribani shilingi Mil. 700, hili hatuwezi kulivumilia tutachukua hatua,” Waziri Ummy.
Ameongeza kuwa Wakurugenzi wa Halmashauri za Same, Bumbuli na Uvinza wanapaswa kujithathimini kwa Halmashauri zao kuchangia asilimia 4 tu ya Bajeti ya Maendeleo kwa mwaka wa Fedha 2020/21.
“Wakurugenzi wa Halmashauri hizi hawafanyi vizuri kabisa mfano Same wamekusanya shilingi mil. 594 ila wametoa shilingi mil. 26 tu kwa ajili ya maendeleo sasa mil. 26 zinafanya kazi gani ya kueleweka?” Waziri Ummy.
Aidha, Ummy ametaja Halmashauri ya Uvinza kuwa imekusanya shilingi mil. 624 na kwenye maendeleo wamepeleka shilingi Mil. 26 tu huku bumbuli ikikusanya shilingi Mil. 336 na kupeleka shilingi Mil.13 tu kwenye miradi ya maendeleo.
Taarifa ya mapato iliyotolewa na Waziri Ummy inaainisha ufanisi wa kila Halmashauri katika ukusanyaji kulinganisha makisio idhinishwa na mapato halisi.
Kwa Mwaka wa Fedha 2020/21 Halmashauri zilipanga kukudanya Shilingi Bil 814.9 kutoka kwenye vyanzo vya ndani na katika kipindi cha Julai,2020 hadi Machi,2021 Halmashauri zimekusanya jumla ya shilingi Bilioni 557.45 sawa 68%.