Wakuu wa nchi mbalimbali za Kusini mwa Afrika wameelezea wasiwasi wao kuhusu hali ya usalama Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), wakisema mashambulizi yanayofanywa na kundi la M23 ni sawa na “ukiukaji wa wazi” wa kusitisha mapigano nchini humo.
Wakiongea kwenye mkutano wa kilele wa dharura uliofanyika Jumamosi mjini Luanda, Angola, wakuu hao walitoa taarifa kupitia Wizara ya Mambo ya Nje ya Angola, ukieleza wasiwasi wake kuhusu kuzorota kwa usalama na hali ya kibinadamu nchini humo.
Pia wameelezea wasiwasi wao kuhusu ripoti kuwa kundi la M23 limeanza tena mashambulizi na kuyakalia maeneo mapya.
Nchi 12 wanachama wa SADC zimeshiriki kwenye mkutano huo uliohudhuriwa na marais wa Angola, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Afrika Kusini, Tanzania, Zambia na Zimbabwe.
Mkutano huo ulisisitiza haja ya SADC kuongoza juhudi katika kukusanya raslimali ili kuhimiza amani na usalama wa kikanda.