Wakati Walimu wakitaja moja ya changamoto inayowakabili kuwa ni riba kubwa za mikopo kwenye taasisi za fedha, benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imeeleza kuhakikisha inaendelea kubuni huduma nafuu za kifedha zitakazosaidia walimu kufikia malengo yao.
Akizungumza katika mkutano wa Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari nchini (TAHOSSA), Meneja wa Benki ya NBC Mkoa wa Dodoma, Happiness Kizigira aMEsema wanatoa huduma za bima za afya, za magari na majengo ambapo mtu anaweza kufanya vitu vyake vikaende salama na inapotokea majanga kupata fidia.
Awali, Rais wa umoja huo, Frank Mahenge alitaja changamoto zinazowakabili walimu ikwemo mikopo yenye riba kubwa inayopunguza ufanisi na kuwakosesha utulivu kazini.
Alitaja changamoto nyingine ni matukio ya kuungua kwa shule, maeneo ya shule kutopimwa, ukosefu wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wakuu wa shule na ukosefu wa usafiri hasa kwa shule za bweni.
“Jambo jingine ukosefu wa vyombo vya usafiri hasa kwa shule za bweni lakini hivi karibuni tulipata changamoto ya baadhi ya shule kuungua moto na shule nyingi kutokuwa na uzio imara hivyo kuhatarisha usalama wa watumishi na wanafunzi,” amesema.
Changamoto hizo huenda zikawa fursa kwa benki ya NBC ambayo tayari ina huduma mbalimbali za elimu ikiwamo bima ya elimu, akaunti za shule pamoja na akaunti za wanafunzi pamoja na mikopo yenye riba nafuu.
“Tulitoa elimu kuwa kuna bima wanazoweza kukatia shule zao ili pindi majanga yanapotokea akaweza kurejeshewa jengo lake. Kwa hiyo muitikio umekuwa mzuri sana na hatutaishia hapa tutatembea hadi katika shule hizo kuhakikisha kuwa kuwa walimu wanapata elimu hii,”amesema.
Aidha, alisema katika kuwasaidia walimu kufikia malengo yao benki hiyo imeanzisha akaunti maalum ya malengo ambayo inawawezesha kujiwekea fedha na kupata riba kila mwezi kwa muda wa mwaka mmoja.
“Tuna pia akaunti za shule na hizi ni mahususi kwa ajili ya shule kwasababu mapato yao ni kidogo hivyo kurahisisha ukusanyaji wao wa mapato kutoka kwa wanafunzi wao. Pia tuna akaunti kwa ajili ya watoto na wanafunzi ambazo hazina makato ya kila mwezi,”amesema.
Mkutano huo umewakutanisha wakuu wote wa shule za sekondari lengu kuu ni kujadiliana, kupanga na kupeana ushauri.