SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) waliwataka wananchi kushiriki katika ‘vita’ ya kutokomeza bidhaa hafifu hapa nchini ikiwa sehemu ya mchango wao wa kumuenzi aliyekuwa Rais wa Tanzania, John Magufuli katika ujenzi wa Tanzania ya viwanda.
Kauli hiyo imetolewa kwa nyakati tofauti na Afisa Masoko wa TBS, Deborah Haule wiki iliyopita wakati wa kuhitimisha kampeni ya kutoa elimu kwa umma katika wilaya ya Musoma, Chato na Karagwe kuhusu umuhimu wa kununua bidhaa zilizothibitishwa na shirika hilo sambamba na kuwahamasisha wafanyabiashara kusajili maduka ya chakula na vipodozi.
Alisema hayati Dkt. Magufuli aliamini mno katika kukuza uchumi kupitia viwanda na TBS wanaahidi kuyaishi maono yake kwa kuhakikisha wanaendelea na juhudi za kuvisaidia viwanda kuzalisha bidhaa bora ili ziweze kukubalika ndani na nje ya nchi kirahisi na hasa zile bidhaa za wajasiriamali wadogo kwani ndo ilikuwa kilio chake kikubwa kwa hawa wadogo kuweza kuingiza bidhaa zao katika masoko ya nje.
“Haya yatawezekana kwa kutoa elimu ya ubora kwa umma na mafunzo ya viwango kwa wazalishaji wadogo sambamba na kuwalea mpaka waweze kukuua na kujisimamia wenyewe katika masuala ya ubora chini ya mpango wetu wa kusaidia wajasiriamali wadogo,” alisema.
Kampeni hiyo ya elimu kwa umma imefanyika katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya shule za msingi na sekondari, masoko, stendi, minadani na maeneo mengine ya wazi ambapo wananchi walijitokeza kupata elimu na ufahamu wa masuala mbalimbali yahusuyo ubora wa bidhaa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Musoma Mjini, Fidelica Gabriel Myovella, aliipongeza TBS kwa kutoa elimu kwa wananchi katika ngazi ya wilaya kwani itaongeza ufahamu na kuhakikisha suala la uuzaji wa bidhaa hafifu sokoni linapungua kama sio kwisha kabisa.
Haule aliwakumbusha wananchi wote kuwa vita ya bidhaa hafifu sio ya TBS pekee bali ni ya Taifa kwa ujumla.
“Kampeni hii imeweza kuwafikia wananchi 14,517 kati yao wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari 12,204 na wananchi 2,313,” alisema Haule.
Haule aliwafafanulia wanafunzi pamoja na walimu umuhimu wa viwango katika maisha yao ya kila siku vile vile kuwafahamisha fursa ya huduma bure kwa wajasiriamali wadogo.
Hata hivyo, aliwaasa wawe mabalozi wazuri wa kuhamasisha ubora katika jamii wanazoishi.
Vilevile aliwasisitiza wananchi kuendelea kutoa taarifa pindi pale wanapokutana na bidhaa zilizokwisha muda wake au wanapotilia shaka bidhaa yoyote katika soko na wafanyabiashara kufuatilia taratibu sahihi za usajili wa bidhaa au majengo kupitia mawasiliano waliyopewa.
Aidha aliwataka kutembelea ofisi ya TBS iliyopo karibu au kupiga simu kupitia kituo cha huduma kupitia mawasiliano waliyopewa.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Musoma Mjini, Fidelica Gabriel Myovella, aliipongeza TBS kwa kutoa elimu kwa wananchi katika ngazi ya wilaya kwani itaongeza ufahamu na kuhakikisha suala la uuzaji wa bidhaa hafifu sokoni linapungua kama sio kwisha kabisa.
Diwani wa Kata ya Bugene wilayani Karagwe, Mugisha Mathias ameipongeza TBS kwa elimu ambayo wanaitoa katika wilaya hiyo kwani kuna baadhi ya wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla hawakuwa na elimu ya ubora wa bidhaa kwa undani zaidi.
“Naipongeza TBS kwa kazi nzuri wanaoifanya na natoa wito waendelee na kasi hiyohiyo ya utendaji,” alisema MMathias.
Kwa upande wake Afisa udhibiti ubora, Mhandisi Emmanuel Shilinde (TBS) aliwakumbusha wauzaji na wanunuaji wa vyakula umuhimu wa kusoma taarifa katika vifungashio na kuuza au kununua bidhaa zilizothibitishwa ubora wake na TBS kwani itawaepusha na hasara ya kupoteza pesa na madhara ya kiafya yatokanayo na utumiaji au uuzaji wa bidhaa hafifu .
Kampeni hiyo itaendelea katika Wilaya za Kilosa, Mkinga na Bagamoyo.