Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan leo tarehe 23 Aprili, 2021 amekutana na kuzungumza na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Dkt. Stergomena Tax ambaye amempa taarifa juu ya masuala mbalimbali yahusuyo SADC.
Mazungumzo hayo yamefanyika Ikulu Jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula.
Katika taarifa yake, Dkt. Tax amempongeza Rais Samia kwa kushika madaraka ya Urais na kuwa Rais wa Kwanza mwanamke Tanzania na amempongeza kwa hotuba nzuri aliyoitoa Bungeni jana ambayo imetoa mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Sita.
Dkt. Tax ambaye anamaliza muda wake wa miaka 8 mwezi Agosti 2021 ameishukuru Tanzania kwa ushirikiano alioupata wakati wote akiwa Katibu Mtendaji wa SADC na ameipongeza Tanzania ambayo wakati wa uenyekiti wake wa SADC imeandaa na kukamilisha mkakati wa maendeleo wa SADC licha kuwepo kwa changamoto za janga la Korono (Covid-19) duniani, imefanikiwa kukifanya Kiswahili kuwa lugha rasmi ya SADC, kuanza mradi wa uwekaji sanamu ya Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere katika Umoja wa Afrika (AU) na uendelezaji wa gesi.
Aidha, amesema katika kipindi hicho SADC imeendelea kuwa na utulivu wa kisiasa ambao umetoa fursa nyingi za maendeleo ya kiuchumi, hivyo ametoa wito kwa Tanzania kutilia mkazo katika uimarishaji wa sekta za uzalishaji kama vile viwanda, kilimo, biashara, kusimamia ubora na kuendeleza miundombinu.
Kwa upande wake, Mhe. Rais Samia amempongeza Dkt. Tax kwa kuiwakilisha vizuri Tanzania katika utumishi wake akiwa Katibu Mtendaji wa SADC na ameahidi kufanyia kazi ushauri na fursa mbalimbali ambazo SADC anazitoa kwa Tanzania.
Mhe. Rais Samia amemkaribisha nyumbani baada ya kumaliza muda wake ili aungane na Watanzania katika ujenzi wa Taifa.