Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia Mwana wa Kifalme Faisal bin Farhan Al Saud.
Rais Samia amemshukuru Mwana wa Kifalme Faisal kwa kufanya ziara hiyo hapa nchini na kwa uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Saudi Arabia ambayo inatoa ufadhili katika kuboresha huduma za afya, elimu, maji na miundombinu hapa nchini.
Amemtaka kufikisha salamu zake kwa Mfalme wa Saudi Arabia Mtukufu Salman bin Abdulaziz Al Saud na kumhakikishia kuwa Tanzania ipo tayari kuendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wake na Saudi Arabia katika Nyanja mbalimbali za kiuchumi na ustawi wa jamii.
Baadhi ya maeneo ambayo Rais Samia ameomba kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano na Saudi Arabia ni kuimarisha biashara ya mazao ya mifugo na uvuvi, mazao ya kilimo, kutumia fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo Tanzania na kuanzisha ofisi ya Ubalozi Mdogo wa Saudi Arabia Visiwani Zanzibar.
Kwa upande wake, Mwana wa Kifalme Faisal amemshukuru Rais Samia kwa uhusiano na ushirikiano mzuri wa Saudi Arabia na Tanzania na amemhakikishia kuwa Saudi Arabia ipo tayari kuuimarisha zaidi uhusiano huo katika maeneo mbalimbali yakiwemo biashara na uwekezaji, na ameeleza kuwa Saudi Arabia inahitaji kupata mazao mengi ya chakula.
Amebainisha kuwa ni muhimu kwa wafanyabiashara wa Tanzania na Saudi Arabia kushirikiana ili kukuza biashara kati ya nchi hizi mbili ikiwa ni pamoja kuwa safari za ndege za moja kwa moja kati ya Tanzania na Saudi Arabia ili kukuza utalii na biashara.
Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula, Waziri wa Uwekezaji Geoffrey Mwambe, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Zanzibar Mhe. Rahma Kassim Ali na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Hamad Masauni.