Walimu na walezi wanaofuata mbinu ya Montessori ni walinzi na watekelezaji wa Sheria ya Mtoto, 2009.
Hivyo watoto ni kipaumbele kwao. Mbinu ya Montessori inawekeza zaidi kwa watoto kati ya mika 2 hadi 6. “Uwekezaji katika miaka mitatu ya mwanzoni, 0-3 ni muhimu zaidi kwa sababu katika muda huo akili zao zinakua kwa asilimia 80 hadi 90,” Bw. Revocatus Sono, mwenyekiti wa MCT.
Katika uwekezaji wa watoto, katika malezi na makuzi yao, ni muhimu kwa walezi hawa wakajali afya zao, ikiwemo afya ya akili. Walezi wa watoto wameshauriwa kutunza afya zao za akili kwa kushiriki katika mambo yanayojenga, kuchagua makundi sahihi ya marafiki, kuwekeza katika upendo: kupenda kazi yako, watoto unaowalea na kuwafundisha. Pia walezi hawa wameaswa kupumzika: kupumzisha mwili na akili na kumtegemea Mungu.
Haya yalizungumzwa na Mr. Cosmas Madulu, mtaalamu wa saikolojia na malezi na Bw. Mosses Raymond, mshauri wa rasilimali watu.
Lakini pia, walimu na walezi wa vituo vya kulelea watoto mchana (day care centres) walionywa na Afisa ustawi wa jamii, Wilaya ya Temeke, Bi. Theresia Nkwanga, kutobaki au kulala na watoto baada ya muda wa shule kuisha (saa 10-12jioni). Na kuwaasa kwamba wanatakiwa kuripoti katika ofisi za serikali ya mitaa na afisa ustawi wa jamii ikiwa wanaona wazazi wa watoto wanachelewa kila wakati kuwachukua watoto wao, kutowajali au kuwafanyia vitendo vyovyote vya ukatili majumbani.
Katibu Tarafa wa Wilaya ya Ilala, Bw. Adrian Kishe, akiwa anaongelea kuhusu malezi ya watoto, alisema kwamba anachukizwa na vitendo vya wazazi kuwapa simu watoto wacheze ‘games’ ili wasiwasumbue, lakini hawarudi pia kukagua ni nini watoto wanakiangalia katika simu hizo.
Akaongeza, “Wazazi mmekuwa busy sana, mkishawapeleka watoto shule mnawaacha, hata hamjui maendeleo yao.”
Mkurugenzi wa MCT, Bi. Sarah Kiteleja aliwaasa walezi kuzingatia malezi ya Kiafrika na kuongeza kwamba mbinu ya kufundishia ya Montessori ambayo inazingatia vitendo zaidi na michezo, inafanana na mazingira ya mtoto wa Kitanzania. Na ili kuwa na malezi bora basi mlezi anatakiwa kuwa bora.