Walimu wawili wa Shule ya Awali na Msingi ya Holly Cross Nursery iliyopo Temeke wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na shtaka la kumuua mwanafunzi wa Shule hiyo.
Washtakiwa hao ni Mkazi wa Gongolamboto, Leahdorice Agunda(35) na Maths Laizer ambaye ni Mkazi wa Mtoni Kijichi.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Yusto Ruboroga kuwa.
Septemba 14, 2020 katika Shule ya Awali na Msingi ya Holly Cross Nursery iliyopo maeneo ya Kijichi Wilaya ya Temeke wote Kwa pamoja walimuua mwanafunzi wa shule hiyo, Catbert Chawe huku wakijua kufanya hivyo ni kosa la kisheria.
Simon alidai upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika hivyo aliiomba mahakama hiyo ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Baada ya maelezo hayo Hakimu Ruboroga alisema washtakiwa hao hawaruhusiwi kujibu chochote kwa kuwa kesi hiyo ni ya mauaji hivyo ameahirisha shauri hilo hadi Novemba 19, 2020.