Walimu wakuu 135 wa shule za msingi wilayani Hanang leo Oktoba 25, 2024 wameanza kushiriki mafunzo maalum ya uongozi na usimamizi wa shule, yaliyofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Nangwa, mafunzo yanayojumuisha mbinu za uongozi, usimamizi wa rasilimali na utekelezaji wa miradi.
Mafunzo hayo, ambayo yamefadhiliwa na serikali kwa kushirikiana na Wakala wa Maendeleo ya Elimu Nchini (ADEM), yanalenga kuwajengea walimu wakuu uwezo wa kitaalamu katika usimamizi wa shule pamoja na kusimamia miradi mbalimbali inayotekelezwa shuleni.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo ya siku tatu, Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu ya Msingi kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Bi. Susan Nussu, amesema mafunzo hayo yanatoa fursa kwa walimu wakuu kuboresha uwezo wao wa kiutawala na kuimarisha utekelezaji wa miradi ya serikali na ni sehemu ya juhudi za serikali kuhakikisha kuwa elimu bora inatolewa kwa wanafunzi kwa kuimarisha mifumo ya usimamizi shuleni.
Kwa upande wake Dkt. Emmanuel Mollel, Makamu Mkuu wa Chuo cha ADEM anayesimamia mipango, fedha na utawala, amewahimiza walimu wakuu kutumia ujuzi watakaojifunza ili kuleta mabadiliko chanya katika shule zao na kuwa mstari wa mbele katika kutekeleza malengo ya serikali ya kuboresha elimu nchini.
Mratibu wa mafunzo hayo, Hashim Issaya, amesema mafunzo haya ni mwanzo wa mkakati mpana wa kuwawezesha walimu wakuu kote nchini kwa watapata mbinu za kisasa ambazo zitawawezesha kuongeza ufanisi na kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora, kwa kushirikiana na wadau wengine wa elimu.