Msemaji wa Umoja wa Mataifa Bw.Stephen Dujarric amesema msafara wa walinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Mali ukiwa na wanajeshi 848 uliokumbwa na milipuko sita na kujeruhi baadhi ya wanajeshi hatimaye umefika eneo la Gao.
Msafara wa kilomita 9 wa malori 143 yaliyobeba wanajeshi na vifaa uliondoka Kidal kaskazini mwa Mali Oktoba 31 wakati kuna hali mbaya ya hewa na kupita kwenye barabara mbovu. Msafara huo umefika Gao Jumanne usiku baada ya kusafiri karibu kilomita 350.
Wanajeshi 37 waliojeruhiwa ama walioruhusiwa kutoka hospitalini wako katika hali nzuri.
Bw. Dujarric alisema hali mbaya ya hewa na ubovu wa barabara ulisababisha magari kuharibika, na kuongeza changamoto ambazo msafara huo ulikumbana nao ukielekea Gao.
Lakini haikujulikana kama milipuko sita ilitokana na mabomu yaliyotengwa zamani na wanamgambo au ni mabomu yaliyolenga msafara huu.